MLINGANO NA MUACHANO KATI YA TAALUMA YA SINTAKSIA NA SEMANTIKI
Katika kujadili mada hili, kwanza tutatoa fasili ya sintaksia na sematikia kama zilivyotolewa na
Wataalamu mbali mbali, kisha tutaelezea na kufafanua kwa kina namna taaluma hizi zinavyojengana au
zinavyohusiana na kuachana, na mwisho tutatoa hitimisho juu ya mjadala huu.
Kwa kuanzia na
taaluma ya sintaksia, wataalamu mbalimbali wameifasili dhana hii kama
ifuatavyo:
Habwe na Karanja (2004) wamesema Sintaksia ni utanzu wa isimu
unaoshughulikia muundo wa sentensi na elementi nyingine zinazounda sentensi
kama vile kategoria za maneno, vikundi na vishazi.
Taaluma ya sintaksia ni tawi mojawapo la isimu linalojishughulisha
na ushambuzi wa namna maneno katika lugha yanavyoweza kufumwa na kuunda vipande
vikubwa zaidi tuviitavyo vishazi, virai na sentensi. (Kipacha, 2007).
Pia, Massamba na wenzake (1999) wamesema Sintaksia ni utanzu wa
sarufi unaojihusishana uchunguzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na
uhusiano wa vipashio vyake.
Hivyo basi, taaluma ya sintaksia
ni tawi la isimu au lughawiya ambalo hujishughulisha na uchambuzi wa maneno
mbali mbali katika lugha jinsi yanavyoungana na kuunda sentensi.
Kwa upande wa taaluma ya semantiki, pia kuna wataalamu mbalimbali
ambao wameweza kufasili dhana hii, miongoni mwao ni:-
Habwe na Karanja (2004) wamesema Semankiti ni utanzu wa isimu unaochunguza
maana katika lugha ya mwanadamu. Wanaendelea kusema kuwa, semantiki hushughulikia
maana katika viwango vyote vya lugha,
kama vile sauti, maneno na sentensi.
Crystal(1987) amesema Simantiki ni utanzu wa isimu unaochunguza
maana katika lugha.
Hivyo basi, taaluma ya semantiki ni taaluma ambayo hujishughulisha
na uchunguzi wa maana katika viwango vyote vya lugha.
Kimsingi taaluma hizi mbili yaani, taaluma ya sintaksia na
semantiki zina uhusiano wa moja kwa moja, hivyo taaluma hizi hujengana na
kutengemeana kwa kiasi kikubwa katika mfumo lugha. Zifuatazo ni hoja na mifano
inayothibitisha na kuonesha mjengano kati ya taaluma ya sintaksia na
semantiki:-
Kwanza, Mjengano hujitokeza katika uainishaji wa
sentensi sahihi na sentensi zisizo sahihi, taaluma ya Sintaksia hutumia kigezo
cha kimaana(semantiki) kama ni kigezo kimoja wapo katika uanishaji wa sentensi
sahihi na sentensi zisizo sahihi. Hili linathibitishwa zaidi tunaporejelea
maana mbali mbali zilizotolewa na Wataalamu kuhusu sentensi kuwa ni “ ni tungo
yenye maana kamili na yenye kjitosheleza.”
Mfano:
a.) Mwalimu anaandika vizuri
ubaoni.
b.) *Yule aliyekuwepo usiku
ule.
c.) *Ungelikuja.
d.) Ali na Juma wanasoma
kitabu.
e.) Anakula.
Katika
mifano hii tunaona kwamba tungo ya (a, d na e) ni sentensi sahihi kwa sababu
zinatoa maana kamili na toshelevu, na tungo zilizobaki (b na c) si sentensi
sahihi kwa sababu haitoi maana kamili. Kwa hiyo kupitia mifano hiyo tunaweza
kuona kuwa taaluma ya sintaksia na semantikia ni taaluma ambazo huweza
kujengana na kutegemeana na kukosekana kwa taaluma moja huweza kupelekea kasoro
katika taaluma nyengine.
Pili, Uhusiano katika mfuatano na
mpangili sahihi wa maneno na viambajengo katika sentensi, Mfuatano na mpangilio
mzuri wa maneno au viambajengo katika uundaji wa sentensi ndio unaosababisha
kupatikana kwa maana sahihi katika
tungo, yaani taaluma hizi zote huzingatia uhusianao na mpangilio mzuri wa maneno katika tungo na kigezo hichi ndicho
kinachosababisha kuundwa kwa sentensi mbali mbali zenye maama kamili.
Kwa
mfano: a.) Mohamed mfupi anasoma
Qur-an vizuri.
b.) *Vizuri anasoma mfupi Qur-an Mohamed.
Katika
mifano ya hapo juu tungo(a) hii ni sentensi sahihi na yenye maana kamili kwa
sababu ya mpangilio mzuri wa maneno katika sentensi hiyo, na tungo (b) hii si
sentensi kwa sababu haijafuata mpangilio sahihi wa maneno na haina maana kamili.
Kwa hiyo, tunapochunguza kwa makini zaidi mifano hiyo hapo juu tunaweza kuona
wazi wazi namna ya taaluma hizi jinsi zinavyokamilishana na kujengana.
Vile vile, uundaji au uzalishaji wa
sentensi mbali mbali katika taaluma ya sintaksia husababishwa na uwepo wa
taaluma ya semankiti. Taaluma ya sintaksia ni taaluma ambayo hushughulika na
uundaji wa miundo tafauti tafauti ya sentensi, lakini kwa kuwepo miundo hiyo
imesababishwa na kuwepo kwa taaluma ya semantiki, yaani kwa kuzingatia kigezo
cha maana tunaweza kuzalisha sentensi mbali mbali kwa kupitia sentensi yenye
umbo moja kwa kuangalia maana ya nje na maana ya ndani ya sentensi.
Kwa
mfano:
“Ali na Salma walizawadiwa na Hassan.”
Katika
sentensi hii, tukitumia kigezo cha kimaana(semankiti) tunaweza kuzalisha
sentensi mbili zenye maana tafauti, kama vile:-
i.)
Ali, Salma na Hassan wote wamepatiwa
zawadi.
ii.)
Ali na Salma ndio waliozawadiwa na
Hassan.
Kwa
hiyo, mifano hiyo hapo juu, inatuonesha namna taaluma ya semantiki inavyosaidia
katika kuzalisha sentensi mbali mbali katika taaluma ya sintaksia.
Mwisho, kanuni ya upatanishi wa
kisarufi, taaluma ya sintaksia lazima izingatia
kanuni ya upatanishi wa kisarufi katika kuunda sentensi yaani izingatia
uhusiano au kuwiyana kati ya kiambishi awali katika jina na kiambishi awali
katika kitenzi, hivyo kanuni hii huathiri taaluma ya semantiki kwa kusababisha
kupatikana kwa maana kamili katika tungo. Na pindipo sentensi inapoundwa bila
ya kuzingatia upatanishi wa kisarufi, vile vile huathiri maana, na huweza
kusababisha utata katika tungo.
Mfano: a.) Mtoto anakula.
b.) *Mtoto wanakula.
Tunapoangalia
mifano hii, tutagundua kwamba sentensi ya (a) imefuata kanuni ya upatanishi wa
kisarufi kwani kiambishi awali “m-” cha
jina kinawiyana na kiambishi awali cha kitenzi ambacho ni “a-” vyote vinaonesha
hali ya umoja, hivyo basi imepelekea kupatikana kwa maana kamili katika
sentensi. Lakini tungo(b) haijafuata kanuni ya upatanishi wa kisarufi kwani
kiambichi awali “m-” cha jina hakiendani na kiambishi awali cha kitenzi ambacho
ni “wa-”, hivyo basi imepelekea kuathiri maana katika tungo hiyo na kusababisha
utata. Kwa hiyo tunapochunguza mifano hiyo, tunaona wazi wazi namna taaluma
hizi zinavyotengemeana na kujengana.
Baada
ya kuangalia namna taaluma hizi zinavyojengana, sasa tutaelezea na kufafanua
namna taaluma hizi zinavyotafautiana yaani kuachana. Taaluma ya sintaksia na
semantiki zinatafautiana katika vipengele vifuatavyo:
Kwanza, katika kigezo cha
uamilifu/kikazi, taaluma ya sintaksia hujishughulisha na kanuni za uundaji wa
sentensi katika lugha, yaani huchunguza namna vipashio vidogo jinsi vinavyoungana
na kuunda kipashio vikubwa na hatimae kuunda sentensi.
Mfano:
i.) neno + neno = kirai
Mwanafunzi
+ hodari =
Mwanafunzi hodari
ii.)kikudi
kirai(KR) + Kikundi tenzi(KT) =
Sentensi
Mwanafunzi hodari +
anasoma = Mwalimu hodari anasoma.
Kwa
upande wa pili, taaluma ya semantiki hujishughulisha zaidi na uchunguzi wa
maana katika lugha, yaani huchunguza maana katika vipengele vyote vya lugha;
sauti, maumbo(maneno) na sentensi.
Mfano;
neno “ota” katika taaluma ya semankiti linaweza kutolewa maana zaidi ya moja;
Ota – kuona picha usingizini
Ota – kuchipuka kwa mmea shambani
Ota – kujipasha, kama vile moto au
jua.
Vile vile, taaluma ya semantiki ni
taaluma inayochunguza maana, na dhana ya maana ni ya kidhahania kwa sababu
maana haina muundo, yaani maana hutengemea zaidi namna ya matumizi katika
jamii(kimazingira au kimuktadha), hivyo maana ya maneno katika lugha huweza
kubadilika kutokana na athari za kimazingira au kimuktadha, isipokuwa maneno
yenye maana ya msingi.
Lakini
taaluma ya sintsksia si dhahania kwa sababu viambajengo vyake hujithihirisha
katika miundo yanayoonekana na kanuni zake katika uundaji haziwezi kuathiriwa
na kimazingira au kimuktadha.
MAREJEO:
Crstal,
D.(1987). The Cambriage Encylopedia of Language.New
York:Oxford University Press
Habwe
& Karanja.(2004). Misingi ya Sarufi
ya Kiswahili. Kenya:Phoenix Publisher.
Kipacha,
A.(2007). Utangulizi Wa Lugha Na Isimu.
Dar es salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.
Massamba,
D. P. B na Wenzake(2001). Sarufi Miundo
ya Kiswahili Sanifu(SAMIKISA). Sekondari na Vyuo. Dar es salaam:TUKI.
Matinde, S. R. (2012). Dafina Ya Lugha Isimu Na Nadharia. Serengeti Educational Publisher:
Tanzania.